Ijumaa , 16th Aug , 2019

Afisa Elimu Vifaa na Takwimu (Sekondari) Manispaa ya Tabora, Bi. Halima Athumani Sangali, ameisifu Kampeni ya Namthamini kwa kujikita kusaidia shule za Vijijini tofauti na ambayo huwa wanafanya wadau wengine.

Wanafunzi wa shule ya Sekondari Ikomwa iliyopo Manipsaa ya Tabora

Bi. Halima ameyasema hayo leo Agosti 16, 2019, wakati akipokea taulo za kike kwaajili ya wasichana wa shule ya Sekondari Ikomwa, iliyopo takribani Kilometa 50 kutoka Tabora Mjini.

"Kampeni hii ya East Africa Television na East Africa Radio nimeipenda sana ni ya tofauti na nyingine, mnafika vijijini kwa wahitaji wenyewe, niwapongeze kwa leo kufika hadi huku Ikomwa ambako huwa hapafikiwi mara kwa mara na wadau" - Amesema Afisa Elimu Bi. Halima.

Afisa Elimu Vifaa na Takwimu (Sekondari) Manispaa ya Tabora, Bi. Halima Athumani Sangali akipokea pedi.

Aidha ameongeza kuwa taulo hizo za kike zitawasaidia wanafunzi kuongeza ufaulu kwani watajikita zaidi kwenye masomo na kuepuka utoro na vishawishi vingine.

Kampeni ya Namthamini ambayo imeshafikia wanafunzi wa kike zaidi ya 5000 ndani ya miaka mitatu, inaendelea kugawa taulo kwa shule mbalimbali ambapo kwa mwaka huu tayari imefika katika mikoa ya Manyara, Arusha na Tabora.