Alhamisi , 10th Oct , 2019

Watu 8 wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime, kwa makosa matano likiwemo la utakatishaji fedha zaidi ya shilingi milioni 234, huku mtuhumiwa mmoja akidaiwa kutoroka.

Hatua hiyo imekuja baada ya kukutwa na mashtaka ya utoroshaji wa madini kinyume na sheria ya madini namba 14 ya mwaka 2010, na kuhujumu uchumi kinyume cha sheria ya utakatishaji fedha sheria kifungu cha 223 ya mwaka 2002.

Akisoma mashtaka hayo Wakili wa Serikali, Anesius Kainunura, ameieleza Mahakama hiyo kuwa mnamo Septemba 22, 2019,  watu hao 8 walikamatwa wakiwa wametenda kosa la kuhujumu uchumi na kukutwa na mawe yenye dhahabu na kufikishwa katika kituo cha polisi.

Kutokana na Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Tarime, kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi na utakatishaji fedha, kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 23, 2019.