Ijumaa , 24th Jun , 2016

Nchi zinazopokea na kuhifadhi wakimbizi zinahitaji kusaidia Jumuiya ya Kimataifa kwa manufaa ya wakimbizi lakini pia wenyeji wanaowapokea ili kuweka mazingira mazuri ya kiusalama na kukua kiuchumi.

Mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa mjini Dar es Salaam nchini Tanzania Alvaro Rodriguez.

Hayo yamesemwa na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa mjini Dar es Salaam, nchini Tanzania Alvaro Rodriguez, na kuongeza kuwa kuna gharama kubwa kwa usalama wa watu na maisha yao na gharama za kiuchumi kwa nchi husika.

Kwa upande wa Tanzania imepokea zaidi ya wakimbizi 140,000 wa Burundi kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja tu kutokana na mtafaruku wa kisiasa nchini humo.

Rodriguez amesema kuwa suala la kupokea wakimbizi linahitaji rasilimali za kutosha ili kuhakikisha watu hawa wanaendelea kuishi maisha yao ya kiutu na ni vigumu sana ukiwa mkimbizi kuweza kujiendeleza kiuchumi kutokana na hali ya ukimbizi.

Ili kuhahikisha hakuna anayesalia nyuma katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu wakiwemo wakimbizi ametoa wito kwa nchi husika kusaidia jumuiya ya kimataifa kuwakwamua kiuchumi wahanga wa ukimbizi ili kufikia malengo.

Ni wito kwa serikali kushughulikia changamoto walizonazo za msukosuko wa kisiasa, wito wa kuchagiza amani kwa jumuiya ya kimataifa, lakini pia ni wito kwa raia wote wa dunia kuelewa kwamba tunapoingia utekelezaji wa maelengo ya maendeleo endelevu, kunahitajika kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma.

Na wakimbizi kuliko mtu mwingine yeyote wanakua na madhila wanapokimbia nchi zao na wanahitaji msaada kutoka nchi zinazowapokea.