Ndege za Tanzania kuwafuata kwao Wachina laki 1

Jumamosi , 17th Nov , 2018

Serikali imewahakikishia watalii nchini China kuwa, wataanza kufuatwa na ndege za shirika la Air Tanzania, na kuwaleta moja kwa koja nchini kwaajili ya masuala mbalimbali ikiwemo utalii na biashara.

Uwanja wa ndege wa Guangzhou

Hayo yameelezwa na Wizara ya Maliasiri na Utalii, kupitia kwa meneja mauzo na usambazaji wa Air Tanzania Edward Nkwambi na Mkurugenzi mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania Devotha Mdachi ambao wamesema lengo la serikali ni kuongeza watalii na wafanyabiashara.

''Tumekuja na mawakala wa Utalii Tanzania hapa Beijing ambapo tuna ziara katika miji 6 na tunauhakika kuwa ifikapo mwezi Februari 2019 idadi ya watalii kutoka China wataongezeka kwani watakuwa na fursa ya kutumia ndege za Air Tanzania moja kwa moja kutokea hapa'', alisema Nkwabi.

Aidha ameongeza kuwa ndege mpya ya kisasa ya 'Dreamliner' itakuwa inafanya safari hizo kutoka Guangzhou hadi Dar es salaam jambo ambalo lazima liongeze idadi ya watalii na kuchocheza ukuaji wa uchumi kupitia biashara kwani China imeendelea kwenye sekta hiyo.

Kwa upande wake Devotha Mdachi amesema Bodi ya Utalii Tanzania inategemea kuona idadi ya watalii kutoka China ikiongezeka kutoka Elfu 30 hadi 60 kwa mwaka na laki moja ndani ya miaka miwili ijayo kutoka na urahisi wa usafiri utakaokuwepo.

Ndege ya Dreamliner ambayo ilinunuliwa na serikali, ina uwezo wa kubeba abiria 240 kwa wakati mmoja na pia ina uwezo wa kufanya safari za moja kwa moja za masafa marefu ikiwemo China na Marekani.