Jumapili , 16th Sep , 2018

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage, amesema kuwa vituo vyote vya uchaguzi katika uchaguzi mdogo unaofanyika hii leo vimefunguliwa kwa wakati sipokuwa kwa vituo vichache sana vilivyochelewa kwa muda wa dakika 10 kutokana na sababu za kiutaratibu.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage.

Jaji Kaijage amesema kuwa hata hivyo zoezi hilo linaendelea katika vituo hivyo vya uchaguzi vilivyochelewa, ambapo pia ameeleza kwamba kulikuwapo na madai kuwa baadhi ya mawakala wamezuiliwa kuingia katika vituo vya uchaguzi.

Amesema kuwa katika uchaguzi mdogo wa Monduli kuna vituo 256 na ni kwenye vituo vinne tu ambapo mawakala wamekataliwa kuingia kwa sababu waliokuja si wale walioteuliwa na vyama vya siasa na kuapishwa na msimamizi wa uchaguzi.

Walikuja mawakala mbadala wengine ambao hawakutimiza taratibu za kuapishwa na waliomba mawakala hao wanne waapishwa hapo hapo kituoni na watu ambao hawana mamlaka ya kuwaapisha,” amesema Jaji Kaijage.

Akiongea katika kituo cha Juhudi kilichopo Ukonga, Jaji Kaijage amesema jimbo la Ukonga kunavituo 673 na zoezi linaendelea vizuri, mwakala wa CCM na Chadema wapo ila mawakala wa CUF hawajaonekana na mawakala hao wamemueleza zoezi linaendelea vizuri na hakuna changamoto ambayo iliyojitokeza.

Mapema leo taarifa toka kwa mbunge viti maalumu ambaye ni msimamizi wa CHADEMA kata ya Esilalei wilayani Monduli, Cecilia Pareso zilidai kuwa mawakala wote wa CHADEMA kwenye kata hiyo wamezuiliwa kuingia kwenye vituo vya kupigia kura kwa kile kilichodaiwa kukosa vitambulisho vya mawakala.

Msikilize hapo chini Jaji Kaijage amefunguka zaidi.