Jumapili , 10th Nov , 2019

Kitu chenye muonekano wa Pembe kilichodaiwa kusababisha wanafunzi kuanguka na kupoteza fahamu wakiwa masomoni, katika Shule ya Msingi Uganga wilayani Makete mkoani Njombe, kimeondolewa shuleni hapo.

Zoezi la kukitoa kitu hicho limeongozwa na Muungano wa Jamii Tanzania (MUJATA), shuleni hapo kufuatia malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wazazi na wanafunzi kuhusiana na kuihusisha shule hiyo na imani za kishirikina.

Akizungumzia kuondoa kwa kitu ambacho kinahusishwa na imani za kishirikina, Mwenyekiti wa Muungano wa Jamii Tanzania (MUJATA), Shayo Masoko, amesema kuanzia sasa shule hiyo ipo shwari na wanafunzi hawatadondoka tena.

Shayo amesema kuwa "hatutamtaja mwenye hiki kitu, hapa sasa pako shwari na kama yupo atakayefanya tena mambo yake hapa shuleni atakipata"

MUJATA kwa kushirikiana na wananchi wa Uganga wamekiteketeza kwa moto kitu hicho, na zoezi hilo limeendeshwa kwa uwazi na kwamba ujio wao shuleni hapo wameletwa na Serikali.