Jumamosi , 16th Apr , 2016

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza amemtumia ujumbe Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, akimhakikishia kuwa hali ya Burundi ni shwari na amemuomba awasihi wananchi wa Burundi warejee.

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza

Barua yenye ujumbe huo, imewasilishwa kwa Rais Magufuli leo tarehe 16 Aprili, 2016 Ikulu Jijini Dar es salaam na Mjumbe Maalum wa Rais Nkurunziza ambaye ni Mnadhimu wa Jeshi la Burundi Meja Jenerali Evariste Ndayishimiye.

Meja Jenerali Ndayishimiye amemueleza Rais Magufuli kuwa Rais wa Burundi Mheshimiwa Pierre Nkurunziza amemtuma kuleta barua hiyo pamoja na shukrani za dhati kwa Tanzania ambayo ni rafiki, jirani na ndugu wa kweli wa Burundi kwa ushirikiano mzuri inaoupata kutoka Tanzania katika masuala mbalimbali.

"Burundi na Tanzania ni ndugu wa kweli, na sisi Burundi tunaiona Tanzania na nchi yetu kama Baba na mtoto wake" amesema Meja Jenerali Ndayishimiye.

Kwa upande wake Rais Dkt. John Pombe Magufuli amemshukuru Rais Nkurunziza kwa kumtumia ujumbe huo na amemhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuwa rafiki na ndugu wa dhati wa Burundi kama ambavyo mahusiano ya nchi hizi mbili yamejengwa tangu zamani.

Kuhusu hali ya Burundi Rais Magufuli amesema anaamini kuwa wasuluhishi mgogoro wa nchi hiyo ambao ni Rais wa Jamhuri ya Uganda Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu wa Tanzania Mheshimiwa Benjamin William Mkapa watafanikiwa kusuluhisha mgogoro huo.

"Naomba umwambie Rais Mhe. Nkurunziza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Burundi, na tunawaombea mgogoro uishe ili muendelee kuijenga nchi yenu" Amesema Rais Magufuli