Nondo alikwenda Iringa kwa mpenzi wake - Mambosasa

Jumanne , 13th Mar , 2018

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa leo Machi 13, 2018 amefunguka na kusema kuwa uchunguzi uliofanywa na jeshi la polisi kuhusu taarifa za kutekwa kwa Abdul Nondo umetoa na kuwa mwanafunzi huyo alijiteka mwenyewe.

Mambosasa amesema hayo wakati akiongea na waandishi wa habari na kusema kuwa Abdul Nondo alikamatwa huko Mafinga Iringa akiendelea na shughuli zake na kusema hakuripoti sehemu yoyote kuhusu kutekwa kwake na kudai kuwa wamebaini kijana huyo alikwenda kwa mpenzi wake ambaye alikuwa akiwasiliana naye mara kwa mara. 

"Pengine alitaka kuzua hilo ili kujipatia umaarufu ila upelelezi uliendelea kubaini kuwa mwanafunzi huyo alikwenda Iringa kwa mpenzi wake ambaye alikuwa akiwasiliana naye mara kwa mara akiwa njiani kuelekea Iringa hii ni baada ya kufanya uchunguzi wa kisayansi na kubaini muda ule aliosema ametekwa simu yake imeendelea kuonyesha mawasiliano aliyokuwa anafanya na huyo binti ambaye alikuwa amemfuata" 

Mambosasa amesema kuwa walipomkamata walikuwa na mashaka kuwa huenda akawa amepatwa na ugonjwa wa malaria ya kichwa iliyopelekea kufanya hayo na kudai kuwa alipelekwa hospitali na kupimwa na kuonekana kuwa mzima asiye na matatizo yoyote ya kiakili. 

"Alikuwa ni mzima wa afya njema na haya aliyafanya kwa makusudi kwa sababu anazozijua yeye mwenyewe, jeshi la polisi limebaini kuwa mwanafunzi huyo alikuwa huru baada ya kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, alisafiri akiwa huru na akafika Iringa akiwa salama, kwa hiyo ni uzushi mtupu uliokuwa na malengo ya hovyo lakini kuna watu wengine walilishabikia jambo hili wengine huwezi kuamini kwa nafasi zao walilishabikia jambo hili la hovyo mtu kujizushia jambo" alisema Mambosasa