Ijumaa , 9th Oct , 2015

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Mhe. Mizengo Pinda amewaonya watanzania wanaobeza juhudi za kuleta maendeleo zilizofanywa na serikali tangu wakati wa uhuru.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Mhe. Mizengo Pinda

Ametoa kauli hiyo jana (Jumatano, Oktoba 7, 2015) wakati akizungumza na wakazi wa Usevya na vijiji vya jirani kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Usevya, wilaya ya Mlele, mkoa wa Katavi.

Alisema ukubwa wa nchi ya Rwanda ni kilometa za mraba 27,000 wakati ukubwa wa Tanzania ni km za mraba 945,000 ambayo ni kubwa mara 35 zaidi ya Rwanda. “Ukubwa wa Rwanda ni sawa na wilaya moja tu ya Mlele ambayo ina ukubwa wa kilometa zaidi ya 29,000. Hivi tuna wilaya ngapi hapa nchini ambazo ni kubwa kuliko Rwanda?, alihoji.

“Acheni tabia ya kulinganisha vinchi vidogo na Tanzania… kazi ya kuleta maendeleo siyo ndogo Tunamhitaji Dk. Magufuli ili aweze kuleta maendeleo kwa kasi hapa nchini kwa sababu yeye ni mchapakazi na kila mmoja wetu anatambua hilo, hataki mchezo na kazi na hata wapinzani wanalitambua hilo,” alisema.

Alisema ameshangaa kusikia watu wakijitapa kuwa watendesha nchi kwa kasi ya ajabu na kwamba ndani ya siku 100 watamaliza shida zote na kuondoa umaskini miongoni mwa Watanzania.

“Kazi ya kuongoza nchi inataka umakini, uzoefu na watu waliobobea kwenye uongozi. Hii si kazi ya majaribio hata kidogo… eleweni kuwa changamoto ni sehemu ya maendeleo. Tuaminini CCM na tupeni nafasi tufanye kazi kwa kumpa kura zote Dk. Magufuli, mbunge wa CCM na madiwani wa CCM,” alisema.

Kwa upande wake, mkuu wa mkoa wa Katavi, Dk. Ibrahim Msengi amewataka wakazi wa mkoa huo wasiwe na hofu na wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura.

“Wote watakaoleta vurugu na kuwazuia wenzao wasipige kura tutawadhibiti sababu tuna nia ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.