Polepole ku-bet suala la CHADEMA kuomba radhi

Jumatano , 5th Aug , 2020

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Hamphrey Polepole amesema kuwa kwa jinsi ambavyo anawajua CHADEMA hawataweza kuwaomba radhi Watanzania, baada ya chama hicho kubadili Beti wa Wimbo wa Taifa na kuufanya kuwa wa chama chao

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Hamphrey Polepole.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Agosti 5, 2020, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, na kusema kuwa jambo la CHADEMA kufanya hivyo limemuumiza yeye pamoja na Watanzania kwani hata CCM inazo nyimbo nyingi lakini haijawahi kuubadili Wimbo wa Taifa 

"Wawaombe radhi Watanzania ila mimi najua hawataomba radhi, kama mnabisha tu-bet hapa, ni desturi yao, nimefanya nao chaguzi nyingi wanavunja sheria, juzi wamemsema vibaya kila mtu kwenye nchi hii, chama hiki ni tatizo kubwa " amesema Polepole.

Aidha Polepole ameongeza kuwa, "Hivi karibuni kulikuwa na mkutano wa chama cha upinzani, hili sikutaka kulisema lakini limetuuma kama Watanzania, juzi naona wenzetu wamebadilisha maneno ya wimbo wa Taifa wameweka maneno ya chama chao, najiuliza mbona sisi CCM, tuna nyimbo nzuri lakini tunaheshimu huu mmoja, hatuwezi kuunajisi kwa kuweka mambo binafsi".