Jeshi la Polisi mkoa wa Morogoro limesema linachunguza tukio la kuchoma moto na kuharibu magari mawili katika wilaya ya Mvomero mkoani humo lililotokea jana Disemba 17, 2025 katika kitongoji cha Kilingeni, Kijiji cha Lusanga, kata ya Diongoya, Tarafa tya Turiani.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro iliyotolewa leo imeyataja magari hayo kuwa ni Mazda CX-5 yenye namba T.214 EJU na Toyota Noah yenye namba T.350 DCH ambayo yalichomwa moto na waombolezaji wa msiba.
“Magari hayo yalitumika kusafirisha mwili wa marehemu Mwanahasan Juma Hamis (18) ambaye ni mfanyakazi wa ndani aliyefariki kwa maradhi jijini Dar es Salaam kisha kusafirishwa Kwenda mkoani Morogoro kwa shughuli za mazishi,”taarifa ya polisi imedokeza.
Hata hivyo, wakati shughuli za mazishi zikiandaliwa ilitokea taharuki iliyohusishwa na kutiliwa mashaka ya mazingira ya kifo cha marehemu hali iliyosababisha kuchomwa ndani kwa magari hayo na kuwafungia ndani wasindikizaji wa msiba ili watoe maelezo zaidi.
Jeshi la Polisi lilifanikiwa kuwaokoa wasindikizaji wa msiba waliofungiwa kwa kushirikiana na uongozi wa serikali ya mtaa na kuanzisha uchunguzi wa kina kuhusu mazingira ya kifo hicho.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kutojichukulia sheria mkononi kwani ni kinyume cha sheria na una madhara makubwa.

