Alhamisi , 18th Sep , 2014

Jeshi la polisi mkoani Dodoma nchini Tanzania limepiga marufuku maandamano ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mkoani humo yaliyopangwa kufanyika leo, ambayo yalilenga kupinga bunge la Katiba linaloendelea mjini Dodoma.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, IGP Ernest Mangu.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma, Emmanuel Lukula amesema kuwa maandamano hayo ni batili kwa kuwa hayako kisheria na kwamba wanapinga kitu kilichowekwa kisheria.

Amesema kama wanataka kupinga maandamano hayo ni lazima wafuate sheria za nchi zilizoliweka bunge hilo na kubainisha kuwa bado kuna mashauri yaliyoko mahakamani ambayo bado hayajatolewa hukumu kuhusiana na kusitishwa kwa bunge hilo.

Katika hatua nyingine, jeshi la polisi makao makuu jijini Dar es Salaam limemuita Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na kauli aliyoitoa hivi karibuni kuwa chama hicho kitafanya maandamano kupinga kuendelea kwa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba.