Alhamisi , 31st Oct , 2019

Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza, linamshikiria kwa mahojiano mwanaume mmoja mwenye  asili ya India, aliyejulikana kwa jina la Yogesh Sumatlal Shah, kwa tuhuma za kukutwa na madini aina ya Almasi yenye thamani ya shilingi milioni 600.

Madini hayo yamekutwa ndani ya begi la raia huyo, aliyekuwa katika harakati za kusafiri kutoka mkoani Mwanza kuelekea Nairobi Kenya, kwa kutumia Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi mkoani humo Jumanne Muliro, amesema baada ya kukamilika kwa uchunguzi, atafikishwa mahakamani kwa mujibu Sheria ya Madini.

Mtuhumiwa huyo ambae anatarajiwa kufikishwa mahakamani, amekutwa na makosa matatu yakiwemo kusafirisha madini bila kibali, kufanya makosa ya kimtandao pamoja na utakatishaji wa fedha.