Rais atangaza hali ya hatari

Jumamosi , 9th Feb , 2019

Rais wa Sierra Leone, Julius Maada Bio, ametangaza vitendo vya ubakaji na unyanyasaji wa kingono kama hali ya hatari kwa taifa.

Rais wa Sierra Leone, Julius Maada Bio.

Tangazo hilo limetolewa juzi baada ya kuwepo malalamiko juu ya kushamiri kwa vitendo vya unyanyasaji wa kingono nchini humo, ambako matukio ya ubakaji yameripotiwa kuongezeka mara mbili zaidi mwaka uliopita na kufikia 8,505 katika nchi hiyo yenye watu milioni 7.5.

Rais Bio amesema baadhi ya familia zinaendeleza utamaduni wa kukaa kimya na kutozungumza kuhusu unyanyasaji wa kingono, hali inayowaacha walengwa wakiwa wameathirika zaidi.

Bio ameongeza adhabu ya hadi kifungo cha maisha gerezani kwa watuhumiwa wa kesi za ubakaji wa watoto wadogo, kutoka adhabu ya kifungo cha miaka mitano gerezani hadi 15.

Takwimu za polisi zinaonesha kuwa theluthi moja ya visa vya ubakaji vilivyoripotiwa vinawahusisha watoto wadogo.