Jumatano , 9th Dec , 2015

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za pongezi kwa watanzania kwa kutumiza miaka 54 kwa uhuru na amani pamoja na umoja.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Katika salamu zake Rais Magufuli amesema kama ilivyokuwa kwa serikali za awamu zilizopita serikali ya awamu ya tano itahakikisha uhuru, amani na umoja wa taifa hauchezewi na mtu kikundi au taifa lolote.

Amesema kuwa taifa litaendelea kuadhimisha kumbukumbu hizo kwa kufanya kazi kwa kuwa wakati tunapata uhuru taifa lilikuwa likiongozwa kwa kauli mbiu ya uhuru na kazi.

Dkt. Magufuli ameongeza kuwa kauli hiyo ilikuwa na lengo la kuamsha moyo na uzalendo kwa kufanya kazi miongoni mwa watanzania kwa kuwatambua kuwa uhuru hautakuwa na maana kama hatutafanya kazi kwa juhudi na maarifa.

Aidha Rais Magufuli amewapongeza viongozi wa mikoa na wilaya na taasisi za umma na binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyojitokeza katika kuhakikisha kuwa zoezi la usafi wa mazingira linafanikiwa.