Jumatatu , 8th Jun , 2015

Rais Jakaya Mrisho Kikwete amezitaka Nchi wahisani kuongeza nguvu katika kusaidia kuendeleza Kilimo nchini Tanzania kwani sekta hiyo ndiyo inayotoa ajira kwa Watanzania wengi zaidi hasa katika maeneo ya vijijini.

Rais Kikwete na waziri mkuu wa Uholanzi

Rais Jakaya Mrisho Kikwete amezitaka Nchi wahisani kuongeza nguvu katika kusaidia kuendeleza Kilimo nchini Tanzania kwani sekta hiyo ndiyo inayotoa ajira kwa Watanzania wengi zaidi hasa katika maeneo ya vijijini.

Rais Kikwete amesema hayo leo tarehe 8 Juni, 2015,  alipofanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi Bw. Bert Koenders.
Rais Kikwete yuko nchini Uholanzi kufuatia mwaliko kutoka kwa Mfalme wa Uholanzi , Mfalme Willem-Alexander. Katika ziara yake ya siku 3, Rais Kikwete anatumia nafasi hii kuishukuru Uholanzi  kwa misaada ya maendeleo  ambayo  imekuwa ikiipatia Tanzania na pia kuwaomba wahisani kuendelea kuisaidia Tanzania hata baada ya  kipindi chake cha uongozi kumalizika.

"Nasikitika sikuweza kubadilisha na kukuza sekta ya kilimo hivyo watu wengi kuendelea kuwa maskini, ni sekta inayojumuisha watu wengi hivyo inahitaji kupewa msukumo  zaidi". Rais amesema na kuongeza kuwa, "Kilimo ni sekta ambayo watu wengi wanaitegemea, lakini haikukua kwa kiwango cha kuridhisha na wala kupewa kipaumbele  inavostahili".

Rais ameongeza na kuelezea jinsi sekta zingine zilivokua katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. "Pamoja na kuendelea kukua kwa uchumi, bado tunahitaji kuongeza juhudi za kupunguza umaskini na ningependa muendelee kutusaidia hasa katika  sekta ya kilimo hata baada ya kuondoka madarakani”.

Rais Kikwete amesema, misaada ya wahisani nchini Tanzania haijapotea kwani juhudi za kukuza uchumi zimefanikiwa kwa kiwango kikubwa ambapo mfumuko wa bei ambao kutokana na msukosuko wa uchumi wa Dunia mwaka 2011 ulifikia asilimia 18.6 na sasa umeshuka hadi  asilimia 4.5 nchini Tanzania.

Hata hivyo Rais  Kikwete amesema sekta ya Kilimo bado inahitaji msukumo zaidi na  kupewa kipaumbele kwa lengo la kupunguza umaskini. "Tunahitaji Kilimo cha kisasa, wakulima kupata mikopo na kujenga maghala" amesema na kusisitiza kuwa hata baada ya kumaliza muda wake wa Urais, ataendelea kuipigania sekta hiyo ili iweze kutoa mchango wake wa kuondosha umaskini wa Watanzania walio wengi.

Waziri Koenders amemuahidi Rais Kikwete kuwa Uholanzi itaendelea kuisaidia Tanzania na kuahidi kuangalia na kufuatilia ombi la Rais Kikwete katika kukuza Kilimo nchini.

Katika mazungumzo yake Mfalme Willem-Alexander na pia Waziri Mkuu Mark Rute, Rais ametoa shukrani kwa misaada ya maendeleo na kuitaka Uholanzi kuendelea kuisaidia Tanzania na pia kuelezea kuhusu uchaguzi ujao ambao Tanzania itachagua Rais wa Awamu ya Tano.

Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
The Haque - Uholanzi
8 Juni, 2015