Alhamisi , 6th Dec , 2018

Rais Dkt. John Magufuli amemteua spika mstaafu, Pius Msekwa kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) na Zakia Meghji kuwa Mwenyekiti wa Braza la chuo hicho.

Rais Dkt. John Magufuli akiwa na spika mstaafu, Pius Msekwa.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Gerson Msigwa imesema kuwa uteuzi huo umeanza leo Disemba 6, 2018, ambapo mbali na hao Rais Magufuli pia amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali wakiwemo wenyeviti na wakurugenzi.

"Rais amemteua Prof. Esnati Osinde Chaggu kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Samwel Gwamaka kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa NEMC", imesema taarifa.

Rais pia amemteua Meja Jenerali mstaafu Michael Isamuhyo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Profesa Gaspar Mhinzi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority (PURA).