Rais Magufuli atuma salamu kwa waziri wa ujenzi

Alhamisi , 30th Jul , 2020

Rais Dkt. John Magufuli amerejea leo Jijini Dar es Salaam akitokea Mtwara baada ya jana kuongoza mazishi ya rais mstaafu wa awamu ya tatu Hayati Benjamin William Mkapa, ambapo akiwa njiani ametoa maagizo kwa Waziri wa Ujenzi kuhakikisha barabara ya Lindi inajengwa katika maeneo yote yaliyo

Rais Dkt. John Magufuli amerejea leo Jijini Dar es Salaam akitokea Mtwara baada ya jana kuongoza mazishi ya rais mstaafu wa awamu ya tatu Hayati Benjamin William Mkapa, ambapo akiwa njiani ametoa maagizo kwa Waziri wa Ujenzi kuhakikisha barabara ya Lindi inajengwa katika maeneo yote yaliyoharibika.

Akiwa njiani rais Dkt. Magufuli amesema kuwa amelazimika kuacha kutumia usafiri wa ndege ili kuweza kutambua changamoto zinazowakabili wananchi katika mikoa ya Mtwara na Lindi ambapo amebaini kuruhusu malori yenye uzito makubwa yanayobeba mawe ya gypsum yameharibu barabara ya Nangurukuru- Lindi.

Amesema kwamba amekerwa na Wizara ya Ujenzi kwa kushindwa kuyafanyia marekebisho maeneo ya barabara yaliyoharibika na kuwahakikishia wakazi wa Somanga kuwa maeneo yote yaliyoharibika yatafanyiwa matengenezo.

“Tunatuma fedha za Bodi ya Mfuko wa Barabara (Road Fund) na tunatuma fedha za Halmashauri haiwezekani Barabara mbovu Kusini hakuna stendi Somanga, Uchaguzi unakuja, tujipange vizuri na tuchague wawakilishi ambao tutawabana na watatuwakilisha vizuri”

Aidha, Rais Dk. Magufuli amesema tayari serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 20 kwa ajili ya kulipa madeni ya wakulima wa korosho na kuwaasa wananchi kuyaenzi yale mema ambayo Hayati Mkapa alifanya ikiwemo kwa kuchapa kazi kwa bidii.

“Tumeshalipa zaidi ya Tsh. Bilioni 800 kwa ajili ya korosho, tumemaliza na hii Tsh. Bilioni 20 (iliyotolewa juzi), tuendelee kushikamana na Serikali yetu na tuendelee kuchapa kazi, Mtwara na Lindi ya sasa sio kama ya kipindi cha nyuma, zinapendeza, zinafurahisha”