Jumamosi , 16th Mar , 2019

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amefanya ziara ya kushtukiza katika mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya Askari Magereza wa gereza la Ukonga Jijini Dar es Salaam na kuagiza mradi huo ukabidhiwe kwa JWTZ.

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo baada ya kubaini kuwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), imeshindwa kutekeleza mradi huo kwa wakati, licha ya serikali kutoa shilingi Bilioni 10 za ujenzi.

Kwa hiyo hapa nisimuone mtu wa TBA, nisimuone mtu wa Magereza kuja kusimamia, muwaache jeshi la wananchi wafanye kazi zao, siku watakapokuja kunikabidhi na mimi nitawakabidhi magereza." amesema Rais Magufuli.

Nataka kila mlipo watu wa Magereza mfanye kazi, msimamie watu, kama ni ng’ombe muwafuge vizuri wazalishe vizuri hadi muuze mazao nje, kama ni kilimo mlime kwelikweli, muwe ni jeshi la kuzalisha."

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameitaka TBA kutoa maelezo ya namna fedha zilizotolewa na serikali kiasi cha shilingi Bilioni 10 zilivyotumika, na ameonya kuwa endapo itabainika matumizi ya fedha hizo hayaendani na kazi zilizofanyika hatua kali zitachukuliwa.