Jumapili , 26th Mei , 2019

Rais mstaafu wa Botswana, Ian Khama amejiengua katika chama tawala kilichoongoza nchi hiyo tangu uhuru miaka 53 iliyopita, akieleza tofauti kubwa baina yake na Rais aliyerithi kiti chake.

Rais mstaafu wa Botswana, Ian Khama.

Khama mwenye umri wa miaka 57, amesema hakuwa na chama chochote lakini ataunga mkono chama cha upinzani cha Umbrella for Democratic Change (UDC) kupambana na chama tawala cha Botswana Democratic Party (BDP). 

Khama aliyeingia madarakani Aprili Mosi 2008 akimrithi Festus Mogae, aliwaeleza maelfu ya wafuasi wake katika mji wa nyumbani kwake wa Serowe jana amesema kwamba alifanya makosa kumteua Mokgweetsi Masisi kuwa rais. 

"Ninaitupa kadi yangu ya uanachama wa BDP, siitambui BDP tena", amesema Khama. 

Maelfu ya watu waliofurika katika mkutano huo pia walirusha kadi zao za BDP. Khama na mrithi wake, Mokgweetsi Masisi  wamekuwa wakilumbana waziwazi kutokana na Masisi kubadili sera zilizoanzishwa na mtangulizi wake, ikiwamo ya hivi karibuni ya kuondoa zuio la uwindani wa tembo.

Hii ni mara ya kwanza kwa Botswana kuona rais mstaafu anakitosa chama hicho tawala.