Rais Mstaafu wa Bunge amtaja anayefuata nyayo zake

Alhamisi , 26th Mar , 2020

Aliyewahi kuwa Rais wa kwanza wa Bunge la Umoja wa Afrika Gertrude Mongella, amemtaja mwanasiasa mwanamke ambaye anaonesha kufuata nyayo zake katika uongozi kuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu.

Rais Mstaafu wa Bunge la Umoja wa Afrika Gertrude Mongella, na Makamu wa Rais wa Tanzania Mama Samia Suluhu.

Mama Mongella ameyabainisha hayo wakati akifanya mahojiano maalum na EATV&EA Radio Digital, na kusema kuwa Makamu wa Rais amekuwa akionesha kuwa imara na kinara tangu akiwa binti mdogo.

"Samia Suluhu nimemuona hata Beijing alikuwepo, kama msichana alikuja na ana uwezo mkubwa sana ni Mama mwenye uwezo mkubwa sana namuombea kwa Mwenyezi Mungu asonge mbele zaidi ni makini na ni mtu mwenye bidii ya kufanya kazi" amesema Mama Mongella.

Gertrude Mongela ameshika nyadhifa mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa, kama kuwa Katibu Mkuu wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Wanawake na kuhudhuria mkutano wake wa nne uliofanyika Beijing, China mwaka 1995.