
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
Akizungumza mara baada ya kuwaapisha Mabalozi hao leo, Ikulu Jijini Dar es Salaam Rais Samia amesema ameainisha baadhi ya mambo anayohitaji kila balozi hao wakayafanyie kazi katika maeneo yao.
"Kwa mabalozi wapya, nakumbuka 27 Julai niliwaeleza wenzenu kwamba jukumu namba moja kwetu ni kuendeleza Diplomasia ya Uchumi ingawa tutakwenda kuipitia sera yetu na kuongeza mengine ambayo kwa wakati huu tutayafanyia kazi," amesema Rais Samia.
"Balozi wetu Italia unatuwakilisha katika mashirika ya Kimataifa, WFP, FAO na IFAD kwahiyo huna budi kuendeleza mashirikiano mazuri. Mfano WFP ni wanunuzi wazuri wa mahindi yetu, ni vizuri uwashawishi wanunue mahindi zaidi,” ameeleza Rais Samia.
Mabalozi walioapishwa leo ni Balozi wa Tanzania Nchini Uturuki Lt. Jen. Yakub Hassan Mohamed, Balozi wa Tanzania nchini Italia Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Marekani Elsie Sia Kanza pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel.