Jumatano , 10th Mei , 2023

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amekikosowa vikali kikosi cha wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kilichotumwa kurejesha amani nchini mwake, akisema mwisho wake ni mwezi Juni.

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Akizungumza kwenye ziara yake ya siku nne nchini Botswana iliyoanza Jumanne (Mei 9), Rais Tshisekedi alidai kuna "usuhuba" baina ya waasi na kikosi hicho cha mataifa ya EAC kilichotumwa nchini mwake mwaka jana, ambako kuna mamia ya makundi ya waasi.

Makundi hayo ni matokeo ya vita vya kikanda vilivyotawala eneo hilo kwenye miaka ya 1990 na 2000, ingawa kwa sasa ni kundi moja makhsusi la M23 ndilo linalotajwa kuwa na nguvu zaidi kuliko mengine.

Kundi hilo kwa haraka lilifanikiwa kuyadhibiti maeneo kadhaa tangu lilipozuka tena mwishoni mwa mwaka 2021 na kuifanya Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye mataifa wanachama saba kuunda kikosi cha kijeshi kukabiliana na hali hiyo mnamo Juni 2022.