Jumatatu , 31st Oct , 2022

Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo amesema nchi yake inakabiliwa na mzozo mbaya zaidi wa kiuchumi kuwahi kutokea nchini mwake.

Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo

Rais huyo amesema katika hotuba yake kwa taifa kwa njia ya televisheni siku ya Jumapili: "Tuko katika mgogoro. Sitii chumvi ninaposema hivyo. Siwezi kupata mfano katika historia wakati vikosi vingi vya nguvu vimeungana kwa wakati mmoja." amesema.

Sarafu ya Ghana Cedi imepungua thamani kwa zaidi ya 50% mwaka huu na imeorodheshwa kama sarafu inayofanya vibaya zaidi duniani dhidi ya dola ya Marekani.

Bw Akufo-Addo alilaumu uvumi na wafanyabiashara haramu wa forex kwa kushuka kwa thamani hiyo, akiongeza kuwa benki kuu itawabana wahusika.

Bei za mafuta zimekuwa zikipanda nchini humo na mfumuko wa bei umepanda na kufikia rekodi ya asilimia 37.2.

Akitangaza hatua kali za kukabiliana na mzozo huo, rais alisema serikali itaendeleza punguzo la asilimia 30 ya mishahara ya rais, makamu wa rais, mawaziri na wateule wengine wa serikali.