Ijumaa , 6th Feb , 2015

Rais  wa Ujerumani  Joachimu  Gauck  aliyekuwa  ziarani  hapa  nchini  ameondoka  kurejea  nchini  mwake   huku  akiwataka  watanzania   kuongeza  jitihada  za  kutunza  rasilimali   za  asili   ikiwemo  hifadhi ya  taifa  ya  Serengeti.

Rais  wa Ujerumani  Joachimu  Gauck alipokuwa akiwasili nchini na mkewe

Akizungumza  kwenye  hafla  ya kumuaga  katika uwanja wa ndege  wa  Kilimanjaro   Waziri  wa  maji  Prof  Jumanne  Maghembe  aliyemwakilisha  Rais  Jakaya  Kikwete  amesema   muda  wote  wa  ziara  Rais  huyo ameelezea  kufurahishwa  kwake  na  ukarimu  wa  watanzania  na  vivutio   walivyonavyo  wakiwemo  wanyamapori.

Katika  hatua  nyingine   mke  wa  Rais  huyo   Daniela  Schadt aliyetembelea   na  Kuzindua  mradi  wa  kusaidia  vijana  unaosimamiwa  na taasisi  ya kijerumani  ya   (DSW)  ulioko Tengeru,   ameshauri   taasisi  zinazosaidia   jamii   kuongeza  jitihada  za  kuwasaidia  vijana   na  kuwajengea  misingi  itakayowawezesha  kusaidia  makundi  mengine   yenye  mahitaji   maalumu  wakiwemo   walemavu  yatima  wajane  na  wazee.

Mkurugenzi wa kituo hicho cha  (DSW) ambacho  husaidia  matatizo mbalimbali   ya  vijana  yakiwemo ya  afya  Peter  Owaga    amesema   pamoja  na  Tanzania  kuwa  na  sera nzuri  bado hazijaweza  kuwasaidia    vijana   tatizo  linaloelezewa  na   waataalam  wa  afya   kama  kikwazo  kikubwa  cha  jitihada  za  kulikwamua  kundi  hilo   na   umaskini.