
Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi
Rais Mwinyi ametoa rai hiyo, leo katika mashindano ya Qur-an yaliyofanyika katika uwanja wa Amani, visiwani Zanzibar ambapo amewahimiza walimu wa madrasa kuendelea kushirikiana na wazee pamoja na Serikali katika kuwaanda watoto kwa kuwapa elimu ya malezi bora kwa kuzingatia maadili na utamaduni wetu.
"Ni vema ofisi ya Mufti kwa kushirikiana na Madrasa zetu ikahakikisha inakuwa na mikakati endelevu ya kuandaa vijana wetu, ili waweze kushiriki na kuwakilishi nchi yetu vizuri katika mashindano ya kimataifa, vijana hawa wenye vipaji watunzwe na waendelezwe ili pale wanaposhiriki waweze kuitangaza vizuri nchi yetu," amesema Rais Mwinyi
Aidha Dkt. Mwinyi ametaka juhudi zinazotumika katika kuwafundisha watoto kuhifadhi Qur-an ziendana na juhudi za kuwafundisha tafsiri qur-an ili kuwajengea misingi imara na kuimarisha imani.
"Tunapowaanda na kulea vizuri watoto wetu matunda yake ni kama haya tunayoyaona leo ambayo yanafaida kubwa kwao, kwetu na vizazi vijavyo, ni vema vilevile juhudi hizi zakuwafundisha watoto kuhifadhi zikaenda sambamba na juhudi zakuwafundisha tafsiri qur-an ili kuwajengea misingi imara na kuimarisha imani ya ucha Mungu" amesema Rais Mwinyi
Awali Rais Mwinyi ameeleza kuwa amani na utulivu uliopo nchini umechagizwa na misingi ya imani ambayo watu wamejengewa ndani ya dini ikiwemo kupendana na kuheshimiana, huku akisema kuwa tunapowaanda vijana kiimani ni hatua muhimu katika kuwaandaa rai wema na kiongozi wadilifu wenye imani na kumkumbuka Mwenyezi Mungu kwa kila wanalo lifanya.