Ajali ya Lori na Costa, mkoani Morogoro.
Awali akitoa taarifa ya ajali hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa, amesema kuwa ajali hiyo imetokea hii leo Agosti 17, 2020 majira ya saa 3:00 asubuhi, baada ya Lori hilo lililokuwa limebeba Tumbaku kupata hitilafu iliyopelekea Tela lake kukatika na hivyo kuziba njia yote, na ndipo dereva wa Costa hiyo alipolivagaa na kuingia ndani ya uvungu wa Tela hilo.
"Tela hilo lilikatika hivyo kusababisha Tela lililokuwa limebeba tumbaku kukata barabara yote na ndipo gari aina ya Costa iliyokuwa ikitoka Dar es Salaam iliweza kuingia ubavuni kabisa mwa hilo Tela, tumeokoa jumla ya watu 6 wamepelekwa Hospitali na hali zao ni nzuri, lakini pia tumetoa watu 4 ambao walikuwa mbele kabisa na walikuwa wamekandamizwa na hali zao ni mbaya" amesema Kamanda Mutafungwa.
Baada ya taarifa hiyo, EATV ilimtafuta Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro Dkt Ritha Lyamuya, ambaye alithibitisha kutokea kwa vifo vya watu 4 vilivyotokana na ajali hiyo.





