Jumanne , 10th Jun , 2025

Askari wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Songwe, wametakiwa kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii ikiwa ni pamoja na kuzingatia maadili ya kazi pindi wanapotekeleza majukumu yao ya kusimamia sheria za usalama barabarani kwa lengo kuendelea kujenga taswira nzuri ya Jeshi la Polisi.

Mkuu wa Operesheni Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Nicholaus Livingstone

Wito huo umetolewa Juni 10, 2025 na Afisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Akama Shaaban, wakati akiwapongeza askari wa kikosi hicho kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya ya kuhakikisha hali ya usalama barabarani inaendeleea kuwepo kwa watumiaji wa barabara Mkoni humo.

"Najua mnatambua moja kati ya maadili ya Jeshi la Polisi ni kufanya kazi kwa kuzingatia utoaji wa huduma bora kwa mteja ambapo ni pamoja na kutumia lugha nzuri wakati mnapowahudumia wateja hao, hii itafanya jamii itoe sifa nzuri na kuendelea kuliamini Jeshi letu," amesema ACP Akama.

Kwa upande wake, Mkuu wa Operesheni Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Nicholaus Livingstone amesema kuwa, rushwa sio maadili ya Jeshi la Polisi na ni kitendo ambacho kinatia doa na kulichafua jeshi hilo pia kinaondoa imani kwa wananchi kwa jeshi hilo hivyo askari wanatakiwa kutojihusisha na vitendo vya rushwa ili kuendelea kuilinda taswira nzuri ya jeshi.