
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule akitoa salamu za pole wa wazazi wa Neema Hoya mwanafunzi wa kidato cha pili aliyefariki katika ajali liyotokea jana Mei 11, 2023 katika Kijiji cha Chidilo Wilayani Bahi iliyowahusisha wanafunzi wa shule ya Sekondari Mpalanga waliokuwa wakielekea shule yaSekondari Magaga kushiriki mashindano ya shule za Sekondari UMISETA.Katika ajali hiyo wanafunzi wawili wamepoteza maisha na wengine 31kujerehuhiwa.
Aidha Senyamule ameahidi kuwa, Serikali itagharamia matibabu ya wanafunzi wote majeruhi 31 walioumia katika ajali hiyo ambao wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Ajali hiyo imehusisha gari yenye namba za usajili T 519 BSY aina ya Mitsubishi Canter mali ya Bw. Abdul Rashid mkazi wa Dar es Salaam. Gari hiyo ilikuwa imebeba wanafunzi 51, walimu wawili na dereva mmoja ambao walikuwa wakielekea Shule ya Sekondari Magaga kushiriki mashindano ya michezo ya UMISETA
Kwa mujibu wa Mkuu wa Usalama barabarani Wilaya ya Bahi, ASP Bakari Ramadhani amesema kuwa, chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari hilo lililobeba wanafunzi, uliosababisha gari kumshinda dereva, kuacha njia na kupinduka na hadi sasa dereva wa gari hiyo anashikiliwa na jeshi la polisi.
Akitoa salamu za Serikali Mhe. Senyamule amewataka wafiwa kuwa na moyo wa subra na kuelekeza Jeshi la Polisi kuchukua hatua haraka kwa wote watakaothibitika kuhusika na uzembe kwa namna yoyote ile.