Jumapili , 26th Jan , 2020

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amesema kuwa Serikali itajenga Mnara wa simu wa TTCL, katika Kata ya Misugha Jimbo la Singida Mashariki kwa lengo la kuboresha Mawasiliano Mkoani humo, kufuatia ombi la Mbunge wa Jimbo hilo Miraji Mtaturu.

Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu

Akizungumza leo Januari 26, 2020 na EATV&EA Radio Digital, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Miraji Mtaturu, amesema kuwa anaishukuru Serikali kwa maamuzi hayo kwani itakuwa mkombozi mkubwa kwa wana Singida katika sekta ya mawasiliano.

"Jana alikuja kuangalia hali ya mawasiliano kwenye jimbo baada ya kumuomba muda mrefu, na akajiridhisha na kuwaelekeza TTCL, na uwekezaji wake ni zaidi ya Milioni 350 na tunatarajia mwishoni mwa mwezi Februari 2020, Mnara huo utaanza kujengwa, na Mnara huo utakuwa ni mkombozi sana kwa ajili ya maendelea ya wananchi" amesema Mbunge Mtaturu.

Jana Januari 25, 2020, Naibu Waziri Mhandisi Nditiye alitembea Jimbo hilo kwa lengo la kujionea hali halisi ya mawasiliano mkoani humo , ambapo alioneshwa kutoridhishwa hali iliyopelekea kutoa maagizo kwa TTCL.