Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania, Dkt Asha-Rose Migiro.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, waziri Dkt Migiro amevitaka vyombo vya habari nchini kutumia nafasi yao kuelimisha jamii, hususani umuhimu wa kuisoma na kuielewa katiba hiyo, ili wafanye maamuzi sahihi wakati wa kura ya maoni inayotarajiwa kufanyika April 30 mwaka huu.
Hata hivyo, zoezi hilo limekosa shamrashamra zilizotarajiwa kutokana na kutokuwepo kwa baadhi ya wadau muhimu katika mchakato wa kutafuta katiba mpya, wakiwemo viongozi wa dini ya Kikristo, vyama vya siasa vinavyounda kundi la UKAWA, pamoja na wawakilishi kutoka Jukwaa la Katiba - JUKATA.
Hata hivyo, wawakilishi wa asasi zilizopokea katiba hiyo wamekuwa na maoni tofauti kwani baadhi wamewataka wananchi kuisoma katiba hiyo kwa makini kabla ya kupiga kura ya maoni.
Mmoja wa waliotoa maoni hayo ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania - MCT, Bw. Kajubi Mukajanga ambaye amesema idadi ya katiba milioni mbili inakidhi haja kwa watu kuisoma na kuielewa.
Hata hivyo baadhi ya wadau wameonesha wasiwasi wao kuhusu muda uliopo kabla ya kupiga kura ya maoni, wakidai kuwa ni mdogo na pengine hautatosha kwa wao kuisoma katiba hiyo na kufanya maamuzi.
Kwa upande wake, Makamu Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Bi. Flaviana Charles amewataka wananchi kutofanya mzaha na badala yake wasome na kujitokeza kwenye kura ya maoni kwani katiba ndio msingi wa uhai wao.