Alhamisi , 25th Mei , 2023

Serikali imesema vifo vya watu wawili vilivyotokea kwa ulaji wa nyama kwenye kijiji cha Msaranga kilichoko Kata ya Kisale, Wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro Mei 4 mwaka huu havihusiani kabisa na ugonjwa wa kimeta.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo (25.05.2023) na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoka kwa Kaimu Mganga Mkuu wa Mifugo Tanzania Dkt. Benezeth Lutege imesema wizara inapenda kuwatoa wananchi hofu na taharuki iliyojitokeza Wilayani Rombo, baada ya majibu ya uchunguzi wa kimaabara kuthibitisha kuwa vifo hivyo havihusiani kabisa na ugonjwa wa kimeta ambao hutokana na kula nyama ya ng’ombe aliyeathirika na ugonjwa huo.

Aidha, taarifa hiyo imebainisha kuwa wizara inawasisitiza wananchi wa Kijiji cha Msalanga, Kata ya Kisale Wilaya ya Rombo na watanzania wote kwa ujumla kuendelea kuchukua tahadhari za kiafya ikiwa ni pamoja na kununua nyama zilizokaguliwa na wataalamu wa mifugo waliosajiliwa na Baraza la Veterinari Tanzania (VCT) na kutoka kwenye mabucha na maduka ya nyama yaliyothibitishwa na serikali kupitia Bodi ya Nyama Tanzania (TMB).

Pia, taarifa hiyo imefafanua kuwa ni vyema wananchi wakajua dalili za ugonjwa wa kimeta ambazo ni pamoja na kifo cha ghafla kwa mnyama aliyeathirika za sehemu zote zilizo wazi hutoa damu ambayo haigandi.

Dalili zingine ni watu ambao hugusana au kula nyama ya mnyama mwenye kimeta, huonesha dalili za homa, kupumua kwa shida, kichefuchefu, kutapika na malengelenge kwenye ngozi dalili ambazo kwa mujibu wa taarifa hazikuonekana kwa wale wagonjwa wawili waliofariki katika tukio hilo.

Taarifa hiyo inabanisha pia ni nadra sana kwa mnyama mwenye kimeta kupatiwa matibabu.