Alhamisi , 16th Aug , 2018

Serikali kupitia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto imesogeza mbele mitihani ya kitaifa katika vyuo vya Afya nchini kutokana na ratiba kuingiliana na sikukuu ya Idd El Haji.

Pichani wanafunzi wakiwa katika chumba cha mtihani.

Kupitia barua iliyotumwa kwa wakuu wa Vyuo vya Afya Tanzania Bara iliyosainiwa na Dkt. Otilia Gowelle, kwa niaba ya Katibu Mkuu Afya ambaye ni Dkt. Mpoki Ulisubisya imesema kuwa imesogeza mbele siku hiyo ambayo ilitakiwa kufanyika Agosti 22, 2018 ili kuhakikisha wanafunzi na watumishi wa sekta hiyo wanapata muda wa kufanya ibada na mapumziko.

Mitihani ya vitendo iliyopangwa ifanyike tarehe 22 Agosti 2018, itafanyika siku inayofuata baada ya tarehe ya mwisho ya mitihani ya vitendo”, imesema taarifa.

Taarifa imeongeza kuwa kutokana na mapumziko hayo itakuwa imeongezeka siku moja kwenye ratiba ya ufanywaji wa mitihani hiyo kwa kada za Afya.