Jumapili , 7th Aug , 2022

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka, ametoa mwelekeo wa kutatua changamoto ya ajira kwa vijana nchini hasa wasomi wa vyuo vikuu huku akitaka wasomi hao watambuliwe na kisha wawezeshwe na hatimaye kujiajiri.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka,

Shaka ameyabainisha hayo alipofanya ziara ya kutembelea maonesho ya kilimo maarufu Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika mkoani Morogoro ambapo amesema kwenye maonesho hayo liko jambo la faraja ambalo ameliona.

"Tumewatembelea vijana wadogo ambao wote na kila mmoja ameweza kutafsiri maono ya Rais kwa aidha kwa kufikiria kuanzisha kitengo cha kuwasaidia vijana wenzake au kuwekeza kwenye masuala haya ya kilimo," amesema Shaka

"Kila mwaka vijana wanahitimu, hivyo nadhani tukiwekeza kwanza kuwa na takwimu sahihi za vijana wangapi wanahitimu lakini pia kuwatambua hao vijana maeneo wanayotoka kisha serikali ikatenga maeneo maalum kila kijana ikampa wastani wa heka japo tano,”alisema Shaka.

Ameongeza kuwa baada ya kutengwa kwa maeneo maalumu  na mashirika ya fedha nayo yakatoa fedha kwa vijana hao anaamini kwa changamoto ya ajira iliyopo wanaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa.