Sheikh aoa mwanaume mwenzake agundua baada ya wiki

Jumanne , 14th Jan , 2020

Sheikh mmoja nchini Uganda aliyejulikana kwa jina la Mohamed Mutumba wa Msikiti wa Kyampisi Masjid Noor, uliopo katika wilaya ya Kayunga, amesimamishwa kufanya kazi hiyo baada ya kumuoa mwanaume mwenzake akidhani ni mwanamke.

Sheikh Mohamed Mutumba na mwanamke feki Swabullah Nabukeera.

Wawili hao waliishi kama mume na mke kwa wiki mbili, bila ya Sheikh kutambua jinsia kamili ya mke wake, ambapo baadae ukweli ulijitokeza baada ya polisi kumkamata mwanamke huyo feki kwa madai ya wizi, wakati wakimfanyia ukaguzi na kugundua alikuwa na jinsia ya kiume.

Akifanyiwa mahojiano na polisi mwanamke huyo feki aliyekuwa akijulikana kwa jina la Swabullah Nabukeera, aliwaambia jina lake kamili ni Richard Tumushabe wala sio Swabullah Nabukeera kama ilivyokuwa ikijulikana. 

Kwa upande wake Sheikh Isa Busuulwa, ambaye ni Imam Mkuu wa Msikiti wa Masjid Noor Kyampisi, amesema kuwa baada ya siku Nne alipokea malamiko kutoka kwa bwana harusi dhidi ya mke wake huyo kukataa kuvua nguo, na kwamba alifikia maamuzi ya kumsimamisha kazi Sheikh Mutumba ili kulinda heshima ya Dini ya Kiislamu.

"Siku nne baada ya harusi yao, Bwana harusi alikuja kulalamika kuwa mkewe alikataa kuvua nguo wakati walikuwa wamelala, nilikuwa napanga kuenda kwao kuwafanyia ushauri kisha nikasikia tena bibi harusi alikuwa amekamatwa kwa wizi wa runinga na nguo za jirani yao" amesema Sheikh Busuulwa.