Alhamisi , 12th Oct , 2017

Jeshi la Polisi kanda maalum Dar es salaam limempa siku 3 tu Sheikh Issa Ponda, ili kujisalimisha na kuhojiwa kuhusu tuhuma zinazomkabili, na iwapo hatafanya hivyo watamchukulia sheria stahiki.

Tarifa hiyo imetolewa leo na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Lazaro Mambosasa alipokuwa akiongea na waandishi wa habari, na kusema kwamba ndani ya siku hizo 3 lazima awe amekwenda kujisalimisha, la sivyo hatakuwa salama.

“Ametenda makosa ya jinai kama uchochezi, lakini pia amekuwa anatoa lugha ambazo ni za kejeli, dhidi ya serikali, anatufutwa na kama unamjua mwambie ajisalimishe ili tuweze kumhoji, kukimbia hakutomsaidia, tukiona kuna kosa la jinai tutampeleka mahakamani kama hana tutamwachia, mimi nampa siku tatu lakini akija leo ni nzuri zaidi, nampa siku 3 ajitokeze mwenyewe aweze kuhojiwa, vinginevyo hatakuwa salama”, amesema Kamanda Mambosasa.

Hapo jana Jeshi la polisi lilivamia mkutano wa Sheikh Ponda aliokuwa nafanya na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, na kufanikiwa kukamata baadhi ya watu wakiwemo waandishi wa habari ambao walikuwepo kwenye mkutano huo.