Sheria kusomeka kingereza, pigo kwa wengi

Ijumaa , 14th Sep , 2018

John Seka aliyewahi kuwa Rais wa zamani wa chama cha wanasheria Tanzania (TLS), ambaye ni wakili wa kujitegemea amesema sheria kuwa katika lugha ya kiingereza si janga la mmoja bali mamilioni ya watu wakiwemo wasomi.

Picha ya ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akiongea na www.eatv.tv,  Seka amesema tatizo hili ni la urithi kutoka zama za kikoloni kwa maslahi yao wenyewe, lakini hadi sasa inatumika kama adhabu kwa wanasheria wenyewe wakati wakiwahudumia wananchi, pia watanzania wanapata shida kuelewa kwani maneno ya kisheria ni magumu sana.

''Kiu ya kujua sheria ni muhimu sana, sheria ndio inayoongoza kila kitu, unaukuta utaratibu mkubwa wa maisha ya watanzania hasa katika nyanja ya sheria unaratibiwa katika lugha ya kigeni ambazo uelewa kwanza wa hata watanzania wanaojua kiingereza ni tatizo, lazima kufanyike jukumu kubwa na watu waanze kujikita kwenye kurahisishaji  uelewekaji wa sheria kwenye lugha nyepesi, na hata kama itakuwa kwa kiswahili iwe kishwahili chepesi''

Aidha ameshauri kwa wale wenye uhitaji wa kisheria kuwatumia wataalam wa sheria pale inapobidi, kwani hata kama ikitafsiriwa kwa kiswahili huenda isieleweke mpaka yule aliyesomea.

''Kama mtu haelewi sheria , anapaswa sasa kuwatafuta hao wanashaeria, mawakili, na wataalam wa sheria kuweza kumwelezea, hao wote ni kazi yao wameshafundishwa kuelezea na kutoa tafsiri kwa lugha nyepesi na inayoeleweka'' ameshauri Seka.

Lakini tayari suala hili limepiga hodi bungeni,  kwani katika bunge la kumi na mbili na kikao cha pili jijini Dodoma ambalo limemalizika leo, mwanasheria mkuu wa serikali Dk. Adelardus Kilangi alitanabaisha kuhususerikali kuwa kwenye mchakato wa kuziandika sheria zote kwa kiswahili japo zoezi hilo linakumbwa na uhaba wa fedha na watafsiri wabobezi wa lugha.

''Sheria ina lugha yake, unapoitafsiri tu moja kwa moja kwenda kiswahili, kuna hatari kubwa pia ya kupoteza mantiki iliyokusudiwa, kwahiyo tuna changamoto pia ya kuwa na wataalam wanaoweza kutufanyia kazi hii kwa usahihii, lakini walau ni kati ya mambo ambayo tumeyawekea mipango tuanze kuyafanyia kazi, sheria zote ziandikwa kwa kiswahili''alitanabaisha Dk. Kilangi