Jumatatu , 8th Mar , 2021

Mkuu wa wilaya ya Kyerwa Rashid Mwaimu, kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Kagera, wamezifungia shule mbili za msingi ambazo ni Kido na Talent kutoa huduma ya bweni, kutokana na majengo yanayotumika kuwalaza wanafunzi kuwa na hali mbaya isiyofaa kutoa huduma hiyo.

Moja ya bweni walilokuwa wakilala wanafunzi

Shule hizo mbili za msingi ambazo usajili wake ni wa kutwa lakini zimebainika kulaza watoto kimya kimya, zimegundulika katika ukaguzi uliofanywa na jeshi la zimamoto na uokoaji kuanzia Februari 05 hadi 23 mwaka huu, unaolenga kubaini kama wamiliki na wasimamizi wa shule wanazingatia kinga ya ajali za moto katika shule.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo Kaimu Mkuu wa jeshi hilo mkoa wa Kagera, Mkaguzi Thomas Majuto, amesema kuwa katika ukaguzi huo baadhi ya shule walikuta zina mapungufu kidogo yanayoweza kurekebishika, lakini nyingine zimekutwa miundombinu yake imeharibika na haifai kulaza wanafunzi.

Mkuu wa wilaya ya Kyerwa Rashid Mwaimu, amewataka wamiliki na wasimamizi wa shule zilizokaguliwa na kubainika kuwa na mapungufu ikiwamo kutokuwa na ving'amua moto na vizimia moto, kutakiwa kubadilisha milango na kuweka milango ya dharura kwa mabweni yenye mlango mmoja, kufanya marebisho hayo katika muda waliopewa, vinginevyo watachukuliwa hatua zaidi.