Alhamisi , 16th Apr , 2015

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Wilfred Soileli, amesema ataungana na jumuiya ya vijana wilaya, katika kampeni yao ya kuwafungia ofisi viongozi wote, wanaoonekana kuwa wasaliti ndani ya chama, kwakuwa wamepoteza sifa za kuendelea kuwa viongozi.

Kuanzia kushoto Aliekuwa Mgombea udiwani wa ccm ndg Mwalimu David Mollel,Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Arusha ndg Wilfred Soileli na Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Arusha.

Soileli ameyasema hayo jana alipokuwa akizungumza, katika hafla ya kumsimika kamanda wa vijana tawi la Osunyai, katika kata ya Sombetini jijini Arusha na kusema, amekuwa akikerwa na tabia ya baadhi ya viongozi hao.

Amesema mbali na kuwafungia ofisi hizo, pia ataanza tabia ya uvunjaji wa kanuni ya kuwaondoa madarakani viongozi hao, pamoja na wanachama ingawa kanuni na taratibu za chama, hazimruhusu lakini itasaidia kuonesha namna anavyokerwa na jambo hilo.

Aidha amesema kwa sasa hawatawavumilia wasaliti na anaungana na jumuiya ya vijana, kuwafungia ofisi viongozi wasaliti, ataanza kuvunja kanuni akithibitisha kuwa msaliti na kumfukuza kazi.

Amesema kwa kipindi kirefu jumuiya hiyo ya vijana, imekuwa ikitaka kutekeleza adhma yao ya kufunga ofisi zote za ngazi zote, ambazo viongozi wake wanaonekana kuwa wasaliti wa chama, lakini yeye na uongozi wa wilaya wamekuwa wakiwasihi vijana hao kutokufanya hivyo.

Ameongeza kadri muda unavyozidi kwenda karibu na uchaguzi, vitendo vya usaliti vimezidi kuongezeka jambo ambalo hata yeye binafsi, linazidi kumkera na hivyo kuona ni bora kazi hiyo ifanyike, ili kuondoa dhana kuwa huwenda hata uongozi wa wilaya nao, unaunga mkono vitendo hivyo vya kisaliti.