Alhamisi , 18th Dec , 2025

Shirika la Masoko ya Kariakoo limekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa makundi mbalimbali ya wafanyabiashara wa soko hilo kwa lengo la kuwasikiliza na kuwapa mrejesho wa namna shirika hilo lilivyoshugulikia maoni na changamoto zao.

Kufuatia ujenzi na ukarabati uliofanywa na Serikali katika soko la Kariakoo ukigharimu takribani Bilioni 28 na kuweka mifumo ya kisasa ya Tehama, usalama, maegesho ya magari pamoja na huduma zingine za kijamii ambayo yanaakisi mifumo masoko ya kisasa duniani, soko hilo litafunguliwa rasmi January 2026.

Wakati hatua hiyo muhimu ikisubiriwa kwa hamu na wafanyabiashara, Shirika la Masoko ya Kariakoo limekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa makundi mbalimbali ya wafanyabiashara wa soko hilo kwa lengo la kuwasikiliza na kuwapa mrejesho wa namna shirika hilo lilivyoshugulikia maoni na changamoto zao.

Meneja Mkuu wa shirika hilo CPA. Ashraph Abdulkarim amewaambia wafanyabiashara kuwa shirika hilo limefanikiwa kuwapangia maeneo wafanyabiashara wa zamani 1520 waliokidhi vigezo vya kurejea sokoni hapo na kupata wateja wapya 351 ambao wameomba kupitia mfumo wa TAUSI.

Ameongeza kuwa kufuatia maoni yao, mkandarasi anafanya marekebisho madogo madogo ambayo yatakamilika mapema iwezekanavyo ili soko hilo liweze kuanza kufanya kazi na kuwafanya wafanyabiashara hao kufanya biashara zao katika mazingira salama na ya uhakika.

Miongoni mwa shughuli zilizofanyika katika mkutano huo ni pamoja na kushughulikia malalamiko ya wafanyabiashara, kusaini mikataba pamoja na kuingiza mikataba hiyo katika mfumo wa TAUSI.