Jumatatu , 21st Mei , 2018

Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu, leo amehudhuria kikao cha Bunge I ikiwa ni mara ya kwanza tangu aachwe huru kutoka jela kwa msamaha wa Rais.

Akiwa Bungeni humo Sugu alipata fursa ya kuuliza swali ambalo lilizua majibizano kati yake na Mwenyekiti wa Bunge Andrew Chenge ambaye ndiye aliyekuwa akiendesha Bunge kwa leo.

Baada ya Sugu kusimama na kuwasha kipaza sauti chake alianza kwa kusema …. “Ahsante Mheshimiwa mwenyekiti, niwatakie mfungo mwema ndugu zangu Waislamu ndani ya Bunge na nchi nzima, kwa wale ambao ni viongozi watumie mwezi huu kujitathimini......(Mwenyekiti akamkatisha na kumwambia “Unaonaje ukiuliza swali”.

Sugu akaendelea kwa kusema.... “Sheria hii pamoja na sheria nyingine mbovu za habari, sio tu inabana kupata habari, pia inatumika kufunga watu jela hovyo kisiasa, mfano mimi nilifungwa kwa kujadili na wananchi wangu taarifa za watu kupigwa risasi, watu kutekwa, watu kuokotwa kwenye viroba, watu kutokuwa na uhuru wa kuongea na kadhalika, kitu ambacho sio mimi tu niliyokijadili, ni kitu ambacho kilishajadiliwa ndani ya Bunge hili, na pia maaskofu wakatoliki ….....Mwenyekiti akamkatatisha na kumwambia “uliza swali...”

Sugu akaendelea.. Swali, ni lini sheria hii itafutwa ili kulinda katiba ya nchi hususan ibara ya 18, mfano.....Mwenyekiti akamkataisha na kumzimia mic akimwambia “ahsante umeeleweka”.

Baada ya hapo Naibu Waziri Mhandisi Edwin Ambandusi Ngonyani alisimama na kuanza kujibu swali la Sugu akisema kwamba sheria zote serikali ina mechanisim ya kuzitazama wakati wowote, na kumtaka kuonana na Mbunge huyo ili waweze kupeana miongozi wapi pana ugumu juu ya sheria hizo.