TAKUKURU yahamia shuleni

Wednesday , 6th Dec , 2017

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini, TAKUKURU, inajiandaa kuanza kutoa elimu ya madhara ya rushwa kuanzia ngazi ya shule ili kuandaa Taifa la baada ye lenye rushwa.

Hayo yamebainishwa leo na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Valentino Mlowola, wakati wa uzinduzi wa utoaji wa huduma kwa umma mjini Dodoma ambapo amesema taifa lolote duniani lenye rushwa halina amani kwa sababu ya wananchi kutofuata utaratibu na sheria za nchi.

“Ili kuwa na taifa la baadaye lisilo na rushwa, TAKUKURU tunajikita kuwekeza nguvu kwa watoto kwa kutoa elimu ya kupambana na rushwa ili kuongeza kasi kubwa ya maendeleo ya nchi na jamii ishiriki katika elimu hii”, amesema Mlowola.

Naye Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Kuboja akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, amesema  serikali ya Tanzania imedhamiria kuidhiirishia dunia kwamba, itasimamima kwa vitendo dhana na misingi ya uadilifu, haki za ubinadamu, uwajibikaji, utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa.

Kwa upande wa Jeshi la Polisi, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Philip Kalangi, amesema dhamira ya Jeshi la Polisi ni kuhakikisha vitendo vya rushwa vinatokomezwa kwenye jamii na raia wote kuishi kwa haki na usawa.