Alhamisi , 7th Dec , 2023

Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga, amewataka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kutobeba changamoto za wakandarasi wabovu na wanaolegalega katika kutekeleza miradi ya usambazaji wa umeme vijijini badala yake wawachukulie hatua kwa mujibu wa mikataba.

Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga

Naibu Waziri Kapinga ameyasema hayo wakati wa ziara yake mkoani Tanga ya kukagua maendeleo ya miradi ya usambazaji wa umeme vijijini katika wilaya ya Korogwe, ambapo pamoja na mambo mengine ameeleza kuwa REA na TANESCO wakibeba changamoto hizo, inasababisha wananchi kufahamu kuwa wao ndiyo wenye matatizo.

Mhe. Kapinga amelazimika kusema hayo kufuatia kuwepo kwa mkandarasi wa Kampuni ya TONTAN kutounganisha umeme katika baadhi ya vijiji na vitongoji vya wilaya ya Korogwe vijijini kwa sababu mbalimbali.

"REA na TANESCO acheni kubeba changamoto za wa kandarasi wabovu na wanaolegalega kwa kuwa wananchi wanaona kuwa ninyi ndiyo wenye shida , msiwakingie vifua wala kuwatatulia changamoto zao hayo siyo matatizo yenu ni matatizo ya mkandarasi asiye muaminifu na hatutakubali  mkandarasi mbovu aturudishe nyuma, TANESCO na REA kazi yenu ni kuwapa kazi wakandarasi na kazi hiyo inatakiwa kuisha desemba 2023 siku chache zimebaki kuanzia sasa", amesema Mhe. Kapinga.

Mkandarasi huyo alitakiwa kumaliza kazi desemba  30 mwaka huu, lakini mpaka sasa takribani siku 24 zimesalia mkandarasi huyo bado hajamaliza kazi, hivyo amewataka REA kutompa kazi tena Mkandarasi huyo hata kama atamaliza kazi hiyo kwa muda uliosalia na Serikali iko kazini kuhakikisha mkandarasi huyo anatekeleza kazi yake kwa mujibu wa mkataba.