Tanga: Askari asafirisha wahamiaji haramu

Jumatano , 12th Mei , 2021

Jeshi la Polisi mkoa wa Tanga linawashikilia raia 7 wa Bangladesh pamoja na Askari Koplo Rashid Mussa wa kikosi cha 835 KJ Kabuku, wakiwa wanatokea Kabuku Handeni kuelekea mkoani Morogoro, ambapo askari huyo ndiye alikuwa dereva wa gari lililokuwa likitumika kuwasafirishia wahamiaji hao. 

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Blasius Chatanda

Akizungumza hii leo Mei 12, 2021, Kamanda wa polisi mkoa wa Tanga Blasius Chatanda,  amesema kuwa tukio hilo limetokea Mei 9 mwaka huu ambapo Askari huyo alikuwa akiwasafirisha watu hao kwa kutumia gari aina ya Noah Alphard lenye nambari za usajili T886 DVX.

Aidha Kamanda Chatanda amesema kuwa bado wanaendelea kufuatilia ili kujiridhisha kwa kuwa hawakuzoea kuwaona wahamiaji haramu wakitokea Bangladesh kupita kwenda Kusini hali iliyowapa wasiwasi kuwa pengine watu hao wanakwenda kujiunga na vikundi vinavyotekeleza uhalifu Kaskazini mwa Msumbiji.