Tanzania yapata kifo cha kwanza cha Corona

Jumanne , 31st Mar , 2020

Tanzania kupitia Wizara ya Afya imetangaza kifo kcha kwanza cha mgonjwa wa Virusi vya Corona, aliyekuwa anapatiwa matibabu kwenye kituo cha matibabu kilichopo Mloganzila Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Taarifa hiyo imetolewa leo Machi 31, 2020 na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na kusema kuwa mtu huyo ni mwanaume na ana umri wa miaka 49.

"Marehemu ni Mtanzania, ana umri wa miaka 49, ambaye pia alikuwa anasumbuliwa na maradhi mengine, Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi, tunatoa pole kwa familia, ndugu jamaa na marafiki" imeeleza taarifa ya Waziri Ummy.

Hadi leo Machi 31, 2020, jumla ya watu waliopata maambukizi ya Virusi vya Corona nchini Tanzania ni 19, na aliyepona ni mmoja na kifo ni kimoja.