Jumapili , 4th Dec , 2022

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na utalii, pamoja na vyombo vinavyojihusisha na wanyamapori na uhifadhi nchini, wameanza zoezi la kuwafukuza Tembo kutoka maeneo ya karibu na makazi ya wananchi na kuwaswaga kuelekea maeneo ya mbugani ili wananchi wawe salama.

Makundi ya Tembo yanayofukuzwa

Zoezi la kuwaswaga Tembo hao kwa kutumia Helikopta limefanyika katika wilaya ya Liwale kutokea wilayani Nachingwea, zoezi linalotajwa kuleta tija baada ya kukamilika, huku baadhi ya wanyama wakifungwa GPS kitaalamu ili wahifadhi waweze kutambua muelekeo wao usiweze kuathiri binadamu.

Nao wananchi wanaeleza namna changamoto ya Tembo ilivyowaathiri, huku wakipongeza zoezi hilo na kuomba lifanikiwe kwani kwa sasa wanashindwa kufanya shughuli zozote za uzalishaji kwa kuwahofia wanyama hao.

Hatua hiyo inakuja kufuatia agizo lililotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, baada ya kupata malalamiko mengi ya wananchi juu ya athari ya wanyama hao.

Wataalamu wanasema, eneo kubwa la hifadhi limeharibiwa na wakulima pamoja na wafugaji waliotia nanga katika misitu minene ambayo sasa inakaribia kuwa jangwa, hivyo ili zoezi la kuwaswaga Tembo hao lifanikiwe kwa asilimia kubwa na wanyama hao wasirudi kwenye makazi ya watu, lazima wizara zinazohusika zichangie kuwaondoa wakulima na wafugaji hao katika eneo la Hifadhi.