Jumatano , 1st Oct , 2025

Takriban watu 60 wamefariki katika tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6.9 katika kipimo cha Richter katikati mwa Ufilipino, wanasema maafisa wa usimamizi wa majanga.

Mji wa Bogo na miji mingine iliyoathiriwa wametangaza 'hali ya maafa' huku wakitathmini uharibifu uliosababishwa na tetemeko hilo.

Tetemeko la ardhi lilitokea kwenye ufuo wa Cebu City siku ya Jumanne na kusababisha kukatika kwa umeme na kuharibu majengo.

Taasisi ya Ufilipino ya Volcanology na Seismology haijatoa tahadhari ya kutokea kwa tsunami.

Wakaazi katika maeneo yaliyokumbwa na tetemeko wamesema kuwa walilala nje mitaani jana usiku

Askofu mkuu wa Cebu amewaambia waumini kukaa mbali na makanisa. Wito huu ni muhimu kwani Cebu kilikuwa mojawapo ya visiwa vya kwanza vya Ufilipino kutawaliwa na Uhispania katika miaka ya 1500, na kina makanisa mengi ya zamani.

Mji wa Cebu, ilioko katika eneo la Visayas, ina wakazi karibu milioni moja.