Ijumaa , 23rd Oct , 2015

Kampuni tatu za maduka ya dawa za binadamu mkoani Mbeya zimeteketeza dawa zilizokwisha muda wake zenye thamani ya shilingi milioni 92 baada ya kuzipeleka kwenye mamlaka ya chakula na dawa TFDA, kanda ya nyanda za juu kusini.

Madawa ya Binadamu

Akizungumza baada ya kuteketeza dawa hizo mkaguzi wa dawa wa TFDA, mkoa Mbeya, Dkt. Silvester Mwidunda amesema kuwa kampuni hizo ziliwajibika zenyewe kukusanya dawa hizo na kuziwasilisha ili ziteketezwe.

Aidha amesema kuwa mbali na dawa TFDA, pia iliteketeza vipodozi vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 8 vilivyokamatwa katika maduka mbalimbali jijini Mbeya.

Kwa upande wake mkaguzi wa mamlaka ya chakula TFDA, kanda ya nyanda za juu Kusini Yusto Wallece amesema kuna changamoto kubwa ya uingizwaji holela wa dawa na vipodozi hali inayochangiwa na ushirikiano hafifu katika mipaka ya Malawi na Zambia.