Ijumaa , 24th Mei , 2019

Waziri Mkuu wa Uingereza, Bi Theresa May ametangaza kuwa atajiuzulu wadhifa wake ifikapo Juni 7, 2019.

Bi May amehudumu katika  nafasi hiyo kwa muda wa miaka mitatu, ambapo amesema muda uliosalia kabla ya kuachia ngazi utumike kwa ajili ya mchakato wa kumpata Waziri Mkuu mpya wa serikali ya nchi hiyo.

Waziri Mkuu huyo anayetokea katika chama cha Conservative amekumbana na ukosoaji mkubwa kutoka kwa miongoni mwa wabunge wake kutokana na mpango wake wa kujitoa katika muungano wa mataifa ya Ulaya, maarufu kama 'Brexit' ambapo ushawishi wake umeonekana kuhusisha vyama vingine.

Katika taarifa yake leo Ijumaa, Bi May amesema kuwa ili kufanikisha mpango wa Brexit, ni lazima mrithi wake aimarishe ushawishi na maelewano mazuri katika bunge.

"Makubaliano hayo yanaweza kufanikiwa tu endapo kila upande ulio katika mdahalo ukiwa tayari kuelewana", amesema Bi May katika hotuba yake.

"Mimi nafanya hivyo bila dhamira yoyote, lakini kwa shukrani kubwa na ya kudumu kuwa na fursa ya kutumikia nchi ninayoipenda", ameongeza.

Naye kiongozi wa chama cha Labour, Jeremy Corbyn, amesema kuwa ni haki kwake kujiuzulu na kusisitiza kuwa  ni wakati sasa wa wananchi wa nchi hiyo kuamua mustakabali wa taifa lao kupitia uchaguzi mkuu wa haraka.