Jumanne , 14th Oct , 2025

Kufuatia kukamatwa kwa Wakili Dastan Mujaki (Roll No. 8016), Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimepinga na kulaani vikali tukio hilo kwani lilikuwa kinyume na taratibu za kisheria.

Taarifa iliyotolewa na Baraza la Uongozi la TLS imeeleza kuwa Wakili Mujaki alikamatwa Oktoba 10, 2025, majira ya saa 2 asubuhi, akiwa ofisini kwake maeneo ya mkabala na Benki ya CRDB Tawi la Bukoba (Kagera) na watu waliodai kuwa ni maafisa wa Jeshi la Polisi ambapo hakuelezwa sababu za kukamatwa kwake.

TLS imesisitiza kuwa hatua ya kumkamata Wakili huyo bila kufuata taratibu za kisheria ni ukiukaji wa haki za msingi za kisheria na kimaadili, ikiwemo haki ya kukutana na wakili wake na viongozi wa Chama chake. Imeongeza kuwa viongozi wa TLS Chapter ya Kagera walipofika Kituo cha Polisi Bukoba kujiridhisha kuhusu hali yake, walinyimwa haki ya kuzungumza naye.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, awali Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera lilisema Wakili Mujaki alikuwa kizuizini akisubiri uchunguzi kukamilika. Hata hivyo, baadaye ilielezwa kuwa alichukuliwa na Kikosi Maalum (Task Force) kutoka Geita, lakini baada ya kufuatiliwa na mawakili wa TLS walioko Geita, ilibainika kuwa hakupelekwa katika kituo chochote cha Polisi katika Mkoa huo.

kupitia taarifa hiyo, TLS imeunga mkono hatua ya viongozi wa Chama hicho 'Chapter' ya Kagera kufungua maombi ya 'habeas corpus' Mahakama Kuu, masijala ndogo ya Bukoba, ili Jeshi la Polisi litoe maelezo rasmi kuhusu mahali alipo Wakili Mujaki na kuhakikisha anafikishwa Mahakamani kupata haki zake.